Photo: UNEP
03 Mar 2022 Tukio Haki na usimamizi wa mazingira

Jinsi Nairobi ilivyokuja kuwa mwenyeji wa makao makuu ya UNEP

Photo: UNEP

Msururu wa vyeti na kumbukumbu zimening'inia kwenye ukuta wa nyuma kwa ofisi ya nyumbani ya Donald Kaniaru, akisherehekea kazi yake na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na Serikali ya Kenya.

Hata hivyo, Kaniaru, ambaye sasa amestaafu, ameweka stakabadhi yake anayoithamini sana kwenye meza yake: nakala ya makubaliano ya kuweka makao makuu ya UNEP jijini Nairobi.

Kuanzishwa kwa UNEP katika mwaka wa 1972 mbali na kufanya maswala ya mazingira kutambulika kimataifa pia ilikuwa mara ya kwanza kwa shirika la kimataifa kuwa na makao yake makuu katika nchi zinazoendelea. Na Kaniaru, wakati huo akiwa na umri wa miaka 30 na akiongoza kitengo cha sheria cha serikali ya Kenya, alitekeleza wajibu muhimu katika uanzilishi wa UNEP.

Kutafuta kuungwa mkono na nchi zinazoendelea

Historia na kuchaguliwa kwa Nairobi kunaweza kuhusishwa na mwaka wa 1965 wakati jiji hili lilipozindua ombi ambalo halikufaulu la kuwa mwenyeji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda. Hali hii lilichochea Nairobi kutumia njia tofauti miaka minane baadaye katika kinyang'anyiro cha kuwa mwenyeji wa UNEP.

“Nilikuwa mmojawapo wa wajumbe wa Kenya wakati huo huku nikimuunga mkono balozi. Azimio ambalo Kenya ilitoa [lilisema] kwamba kutokana na makao makuu mengine kuwa Amerika Kaskazini na Ulaya Magharibi, kunapaswa kuwa na usawa," Kaniaru anasema.

Kaniaru anasema Kenya "iliandamana" na "na kukaza kamba," hali iliyofanyasha Umoja wa Mataifa kutuma kikosi chake kutathmini Nairobi. 

“Nilitumwa Nairobi mara moja alasiri hiyo kukutana na kikosi hicho. Serikali ya Kenya ilikuwa imefanya mashauriano ya ngazi ya juu zaidi.  Kwa hivyo, iliwezekana [kutatua] wasiwasi wowote."

Wakati uo huo, Kenya ilifanikiwa kuungwa mkono na mataifa mengine yaliokuwa yametuma maombi ya kuwa wenyeji wa makao makuu ya UNEP, ikiwa ni pamoja na Mexico City na New Delhi. Kutokana na umoja huu, ombi la Nairobi lilipitishwa rasmi tarehe 15 Desemba mwaka wa 1972 wakati wa kikao cha 27 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambacho kilihusisha Nchi zote Wanachama. Ombi hili lilipigiwa kura 128 kuliinga, hakuna aliyepinga wala aliyezuzia. 

"Historia iliwekwa," Kaniaru anasema. "Hivyo ndivyo hii taasisi ilijikuta Nairobi, Kenya."

UNEP sign
Makao Makuu ya UNEP' kwa sasa. Picha: UNEP

Kuanza kazi

Baada ya kukabidhiwa ombi lao, Kaniaru na kikosi chake waliendelea kujitolea kuhakikisha UNEP itatua haraka katika makao yake makuu mapya. Kufikia Oktoba mwaka wa 1973, UNEP ilikuwa imeanzisha ofisi katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta. Miaka miwili baadaye, ilihamia katika eneo jipya kwenye shamba kuu la kahawa viungani mwa Nairobi, ambako imesalia hadi leo. 

“Kenya ilijitolea kabisa. Makubaliano kuhusu makao makuu yalikubalika haraka - ulikuwa uamuzi wa haraka zaidi kuwahi kuchukuliwa popote kuhusiana na makao makuu yoyote," anasema. "Ilikuwa fursa nzuri sana. Kulikuwa na furaha kubwa.” 

Furaha anayoizungumzia Kaniaru bado haijabadilika miaka hii yote baadaye: anapoendelea kusimulia hadithi yake, anatabasamu anapoongea. 

"Ilihisi kama tulikuwa tukitoa fursa ya kwanza ya aina hii katika nchi zinazoendelea. Na bila shaka, ni miaka 50 tangu UNEP ipate makao yake makuu ya kujivunia katika sehemu hii ya dunia.” 

Kaniaru alijiunga na UNEP mwaka wa 1975, ambapo alishikilia nyadhifa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Utekelezaji wa Sera ya Mazingira, hadi kustaafu kwake miongo mitatu baadaye.

Baada ya miaka 50 ya kuwepo kwake, Kenya bado inaichukulia UNEP kama shirika la kipekee katika Mfumo wa Umoja wa Mataifa ambalo linatoa fursa kwa Afrika kuelezea changamato zake za mazingira na kushirikisha ulimwengu kupata masuluhisho kupitia vitendo.  

"UNEP ni ya thamani. Ni gari ambalo sisi tunaoishi Afrika tunaweza kuelezea wasiwasi wetu kuhusu uendelevu wa mazingira,” anasema Balozi Rachelle Omamo, Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Kenya.

Muda unavyosonga, UNEP imethibitisha kuwa jukwaa linaloitisha mikutanao ili kuangazia masuala ya kimataifa ya mazingira na kupigania kuchukuliwa kwa hatua madhubuti.

Tulianzisha kile ambacho sasa, kwa maoni yangu, ni hadithi iliyo na mafanikio sana na shirika lililo na mafanikio. 

UNEP@50

Kufuatia Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa 5,2 (UNEA 5,2) – taasisi ya ngazi ya juu zaidi ya kufanya maamuzi kuhusu mazingira - kikao maalum kinachojulikana kamaUNEP@50 kitafanyika Nairobi kuanzia tarehe 3-4 Machi ili kuadhimisha miaka 50 ya kuwepo kwa UNEP.

Kikao hiki kinatoa fursa ya kuimarisha tena ushirikiano wa kimataifa na kuchochea hatua za pamoja za kushughulikia changamoto za aina tatu duniani za mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira na bayoanuai, na uchafuzi na taka. 

UNEP inapokaribisha viongozi wa dunia na wawakilishi kutoka Nchi Wanachama mjini Nairobi, Kaniaru anasema ni muhimu kutafakari juu ya siku zilizopita na kufikiria kuhusu miaka 50 ijayo - na zaidi - kuhusu uhusiano muhimu wa UNEP na Nairobi, Kenya na nchi zinazoendelea. 

"Tulianzisha kile ambacho sasa, kwa maoni yangu, ni hadithi iliyo na mafanikio sana na shirika lililo na mafanikio," Kaniaru anasema. “Kisa hiki ni cha matumaini na kuwa na mustakabali bora.”

 

Maudhui Yanayokaribiana