pixabay
08 Dec 2023 Toleo la habari Kushughulikia Mazingira

Kutumia bidhaa mpya mbadala badala ya nyama na maziwa kunaweza kusaidia kupunguza uzalishaji wa hewa chafu inayodhuru - Umoja wa Mataifa

Dubai, Desemba 8, 2023 - Bidhaa mpya mbadala zinazoibuka badala ya bidhaa kutoka kwa wanyama kama vile nyama na maziwa zinaweza kuchangia pakubwa kupunguza athari kwa mazingira za mfumo uliopo kwa sasa wa chakula duniani, hasa katika nchi za kipato cha juu na cha kati, mradi zikitumia nishati ya kiwango kidogo cha hewa ya ukaa. Haya ni matokeo muhimu ya tathmini mpya ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) ya bidhaa hizo mpya mbadala za kilimo cha ufugaji wa wanyama, sekta inayochangia humsi ya uzalishaji wa hewa chafu, huku ulaji wa nyama ukitarajiwa kukua kwa asilimia 50 kufikia mwaka wa 2050. 

Ni kipi kinachoendelea? Tathmini ya athari zinazoweza kutokea kutokana na masuluhisho mapya yaliyochaguliwa badala ya bidhaa za kawaida kutoka kwa wanyama inaangazia bidhaa tatu mbadala: 1) Bidhaa mpya za nyama kutoka kwa mimea, 2) Nyama iliyotengenezwa kutoka kwa seli za wanyama, na 3) Bidhaa zenye protini nyingi zinazotokana na uchachishaji wa haraka unaofanywa na vijidudu. Ni sehemu ya msururu wa ripoti za Mipaka za UNEP, zinazotambulisha na kushughulikia masuala ibuka yanayoathiri mazingira.

Ripoti hii, iliyotolewa kwa ushirikiano na Serikali ya Ubelgiji, inaonyesha kuwa bidhaa hizi mbadala mbali na kuwa na uwezekano mkubwa wa kupunguza uzalishaji wa gesi chafu (GHG), pia zinaweza kuchangia kupunguza uharibifu wa ardhi na ukataji miti, uchafuzi wa maji na udongo na uharibifu wa bayoanuai, mbali na kupunguza hatari za magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama na vimelea sugu dhidi ya madawa. Hizi bidhaa mpya mbadala zinaweza pia kusaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa wasiwasi kuhusu maslahi ya wanyama, ikilinganishwa na bidhaa za kawaida.

Waandishi wanahitimisha kwa kusema kuwa bidhaa mpya zinaweza kutekeleza wajibu wa kusaidia kuwepo na mfumo wa chakula endelevu zaidi, wenye virutubishi zaidi na wa kiutu zaidi, unaotofautiana kutegemea kanda. Hupitia sera ambazo watoa maamuzi wanaweza kuzingatia ili kuwa na utoshelezaji wa chakula, ajira, riziki, usawa wa kijamii na kijinsia, na utamaduni wa kusaidia kuimarisha manufaa ya nyama na maziwa mbadala, huku tukiepuka athari mbaya kwa afya na jamii zinazoweza kutokea. 

"Bidhaa mbadala vya chakula vitaongeza bidhaa zinazoweza kuchaguliwa za watumiaji," Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP alisema. "Zaidi ya hayo, Bidhaa mbadala kama hizi zinaweza pia kupunguza shinikizo kwa ardhi ya kilimo na kupunguza uzalishaji wa gesi chafu, na hivyo kutusaidia kushughulikia changamoto za aina tatu duniani - janga la mabadiliko ya tabianchi, janga la uharibifu wa bayoanuai na mazingira, janga la uchafuzi na taka - na vile vile kushughulikia athari za kiafya na kwa mazingira za sekta ya ufugaji wa wanyama. Usaidizi zaidi kutoka kwa serikali, pamoja na utafiti wazi unaofanywa kwa njia za wazi, vinaweza kusaidia kuonyesha uwezo wa teknolojia hizi mpya kwa baadhi ya nchi."

 Ingawa bidhaa za kawaida kutoka kwa wanyama ni chanzo muhimu cha protini kwa jamii nyingi, hasa katika nchi zinazoendelea, katika nchi nyingi za kipato cha juu na cha kati, uzalishaji na matumizi yake hutokea kwa kiwango ambacho huathiri vibaya watu na sayari.  Mabilioni ya wanyama wanaochinjwa kila mwaka sio tu waathiriwa wa pekee wa sekta ya kilimo cha ufugaji wa wanyama inayokua kwa kasi. Uzalishaji na utumiaji wa vyakula vinavyotoka kwa wanyama, huku vikitoa virutubishi muhimu, pia umehusishwa na madhara makubwa kwa afya ya umma: ulaji wa nyama iliyochinjwa na iliyosindikwa kwa viwango vya juu  huhusishwa na magonjwa ya moyo na mishipa, aina fulani ya saratani, kunenepa kupita kiasi, na kisukari. Kilimo cha kufuga wanyama pia kinahusishwa na ongezeko la vimelea sugu dhidi ya madawa - asilimia 73 ya dawa zote za kuua vijidudu zinazouzwa hutumika katika kilimo cha ufugaji wa wanyama - na kuenea kwa magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kama vile COVID-19 au Influenza aina ya Avian.

Sekta ya kilimo cha ufugaji wa wanyama ni kichocheo kikuu cha mabadiliko ya tabianchi: uzalishaji wa gesi ya ukaa kutoka kwa wanyama, uzalishaji wa chakula, mabadiliko ya matumizi ya ardhi na usambazaji mwingi wa nishati duniani huchangia angalau asilimia 60 ya uzalishaji wa GHG unaohusiana na chakula na asilimia kati ya 14 na 20 wa uzalishaji wa GHG duniani.

Ingawa vyakula vipya mbadala vinaweza kupunguza madhara kwa wanyama wanaofugwa na vinaweza kuchangia kuboresha afya ya umma, manufaa mengine ya kiafya si dhahiri: baadhi ya bidhaa mpya zinavyotokana na mimea hukulika kwa urahisi na huwa na kiasi kikubwa cha chumvi na mafuta mazuri. Ushahidi kuhusu athari kwa afya za kutumia nyama iliyotengenezwa kutoka kwa seli za wanyama au uchachishaji ni chache mno. Kwa kuiga kwa karibu au kufuata mfumo wa nyama na bidhaa nyingine kutoka kwa wanyama, bidhaa mbadala zinaweza kusaidia watumiaji, hasa katika nchi za kipato cha juu na cha kati, kuachana na viwango vya juu vya matumizi ya protini za wanyama kwa njia siziso endelevu. Hata hivyo, gharama, ladha, na kukubalika kijamii na kitamaduni kutaathiri pakubwa mwelekeo wa njia mbadala za asili za bidhaa za wanyama za kawaida.  

Ripoti hii inasisitiza kuhusu umuhimu wa kuhakikisha kuna mabadiliko ya haki kupitia njia mwafaka kuzingatia kanda kwa mabadiliko ya mifumo ya chakula. Inapitia sera zinazoweza kutumika kubadilisha sekta ya chakula kuwa na mustakabali mzuri na endelevu zaidi: msaada mkubwa ili kufikia utafiti na kufanya biashara kwa njia ya wazi, kubadilisha ruzuku, kupunguza ushuru, uwekezaji wa moja kwa moja wa kifedha, na dhamana ya mkopo ipendelee bidhaa mpya mbadala, pamoja na mifumo iliyokubaliwa kimataifa kuhusu sera nzuri za biashara na viwango vya usalama wa chakula. 

Waandishi wanasisitiza kuhusu utafiti wa wazi unaofanywa kwa njia ya wazi ili kuelewa athari za matumizi ya mara kwa mara ya kula bidhaa mbadala, na kuelewa athari kwa jamii na kwa uchumi za matumizi yake katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na usawa, utoshelezaji wa chakula, na mapato ya wakulima wadogo.

Ripoti haizingatii nyama kutoka kwa wanyama pori, samaki au wanyama wengine wa majini, ingawa teknolojia mpya zinaweza pia kuleta mabadiliko katika sekta ya uvuvi. Ripoti hii si tathmini ya njia nyingine mbadala kwa mfumo wa sasa wa chakula: mashamba ya kisasa ya mifugo, kuongeza kwa chakula vitu vya kupunguza uzalishaji wa hewa chafu kutoka kwa kilimo cha kufuga wanyama, wadudu wanaofugwa, kupunguza ulaji wa nyama na kutumia protini kutoka kwa mimea kama vile maharagwe, bidhaa za wasiokula nyama kama vile tofu, au kutoza nyama ushuru. Bidhaa hizi mbadala tayari zinafuatiliwa mbali na bidhaa tatu mbadala zilizotathminiwa katika ripoti hii, lakini zimeshindwa kufikia sasa kupata usaidizi wa serikali na kupata athari kwa kiwango au kasi inayohitajika.

 

MAKALA KWA WAHARIRI

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)

UNEP ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira duniani. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.

 

Kwa mawasiliano na vyombo vya habari, tafadhali wasiliana na:

Taarifa ya Habari kutoka UNEP: unep-newsdesk@un.org