Unplash/Marcin Jozwiak
26 Apr 2022 Toleo la habari Vichimbuaji

Matumizi yetu ya mchanga "yametufinyia kwenye ukuta", inasema ripoti ya UNEP

  • Tunahitaji utambuzi wa kimkakati wa mchanga na kuchukua hatua katika sekta zote zinazohitajika, ripoti yahimiza    

Geneva, Uswisi, Aprili 26, 2022 – Tani bilioni 50: zatosha kujenga ukuta wenye upana wa mita 27 na urefu wa mita 27 kuzunguka sayari ya Dunia.  Hiki ni kiwango cha mchanga na changarawe kinachotumika kila mwaka, na kuifanya kuwa rasilimali ya pili inayotumika zaidi duniani kote baada ya maji.  Kwa kuzingatia tunavyoutegemea, mchanga unapaswa kutambuliwa kama rasilimali ya kimkakati na uchimbaji na matumizi yake yanahitaji kufikiriwa upya, inavyoonyesha ripoti mpya ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP). 

Mchanga ni rasilimali ya pili duniani kwa matumizi na unapaswa kusughulikiwa viziri  Mabadiliko ya kisheria, nyenzo za ujenzi kutoka kwa vitu vilivyotumiwa, mawe yaliyopondwa na ‘mchanga wa madini’ kutoka kwa uchimbaji wa madini, ni miongoni mwa masuluhisho.  

Ripoti hiyo, Mchanga na Uendelevu: Mapendekezo 10 ya kimkakati ya kuepusha janga, iliyotolewa leo na kikosi cha UNEP’s GRID-Geneva, inatoa mwongozo unaohitajika uliokusanywa kutoka kwa wataalamu duniani ya kuanza kutumia mbinu zilizoboreshwa za uchimbaji na usimamizi wa rasilimali hiyo.

Kuchimba mchanga ambako una umuhimu mkubwa kwa mifumo ya ekolojia, kama vile mito, maeneo ya pwani au baharini, kunaweza kupelekea mmomonyoko wa udongo, kuongezeka kwa chumvi kwenye chemichemi ya maji, kupoweza kustahimili mawimbi ya dhoruba na athari yake kwa bayoanuai na kuhatarisha maisha kupitia, usambazaji wa maji, uzalishaji wa chakula, uvuvi, au sekta ya utalii na kadhalika. 

Kwa mjibu wa waandishi wa ripoti hiyo, mchanga ni sharti utambuliwe kama rasilimali ya kimkakati, sio tu kama nyenzo ya ujenzi, lakini pia kwa kwa kaxi zake mbalimbali kwa mazingira.  Wanasisitiza kuwa serikali, viwanda na watumiaji wanapaswa kuweka bei ya mchanga kwa njia ambayo inatambua thamani yake halisi katika jamii na kwa mazingira.  Kwa mfano, kuweka mchanga ufuoni unaweza kuwa mkakati wa gharama nafuu zaidi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kutokana na jinsi unavyolinda dhidi ya mawimbi ya dhoruba na athari yake kutokana na kupanda kwa kina cha bahari - huduma kama hizo zinapaswa kujumuishwa wakati wa kukadiria bei yake. 

Kiwango cha kimataifa kuhusu jinsi ambavyo mchanga unavyochimbwa kutoka kwa mazingira ya baharini pia kinapaswa kuwekwa, ripoti hiyo inapendekeza.  Hii inaweza kuleta mabadiliko makubwa chanya kwani uchimbaji mwingi wa baharini hufanywa kupitia zabuni za umma zilizo wazi kwa kampuni za kimataifa.  Wakati uo huo, ripoti hiyo inapendekeza kwamba uchimbaji wa mchanga kutoka fukweni upigwe marufuku kutokana na umuhimu wake kwa ustahimilivu wa maeneo ya pwani, mazingira na uchumi.

 "Ili kufikia maendeleo endelevu, tunahitaji kubadili kwa kiwango kikubwa namna tunavyozalisha, namna tunavyojenga na kutumia bidhaa, na kubadili miundombinu na huduma zetu.  Rasilimali zetu za mchanga huisha, na tunahitaji kuzitumia kwa njia ya busara.  Tukielewa jinsi ya kushughulikia nyenzo dhabiti zinazochimbwa zaidi ulimwenguni, tunaweza kuepuka janga na kukuza uchumi unaotumia rasilimali zaidi ya mara moja," Pascal Peduzzi, Mkurugenzi wa GRID-Geneva kwa UNEP na mratibu wa jumla wa programu wa ripoti hii.

Miundomsingi, nyumba, chakula na mazingira yamo hatarini 

Mchanga ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na unahitajika kutengeneza saruji na kujenga miundomsingi muhimu kuanzia kwa nyumba na barabara hadi kwa hospitali. Kwa kutoa makazi na maeneo ya kuzaliana kwa mimea na wanyama mbalimbali, mchanga pia una umuhimu mkubwa wa kusaidia bayoanuai, ikijumuisha mimea ya baharini inayoteka kaboni au kuchuja maji.  Rasilimali hiyo ni muhimu ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu na kukabiliana na majanga ya aina tatu kwa sayari ya mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi na uharibifuwa bayoanuai.  Hata hivyo, inatumika kwa kasi kuliko inavyoweza kujitengeneza tena, na kwa hivyo  kuwajibika kuusimamia ni muhimu.

Uchumi unaotumia bidhaa tena na tena  

Waandishi hao wanabainisha kuwa kuna masuluhisho ya kuwezesha kuwa na uchumi unaotumia mchanga tena na tena, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku utupaji wa taka za madini na kuhimiza mchanga kutumika tena wakati wa kutoa zabuni kwa umma ni miongoni mwa hatua za kisera zilizotajwa.  Miamba iliyopondwa au nyenzo za ujenzi na vitu kutokana na ubomoaji zilnazotumiwa tena, pamoja na ‘mchanga wa madini’ kutoka kwenye machimbo ya madini ni miongoni mwa vitu mbadala mwafaka vya kutumiwa badala ya mchanga ambavyo pia vinapaswa kutolewa ruzuku, ripoti hiyo inaeleza.

Wanaongeza kuwa miundo mipya ya kitaasisi na kisheria inahitajika ili mchanga uweze kushughulikiwa kwa ufanisi zaidi na mbinu bora zitumiwe na kutekelezwa.  Rasilimali za mchanga lazima zaidi ziorodheshwe, kufuatiliwa na ripoti kutolewa, ripoti hiyo inapendekeza.  Wakati uo huo, wadau wote lazima wahusishwe katika maamuzi yanayohusiana na ushughuliaji wa mchanga ili kuruhusu mbinu zinazotegemea eneo na kuepuka umasuluhisho yaleyale kwa kila eneo, ripoti inasisitiza. 

Ripoti hiyo inafuatia azimio la Usimamizi wa rasilimali za Madini lililopitishwa katika Mkutano wa nne wa Baraza la Mazingira la (UNEA) uliotaka kuchukuliwa kwa hatua za usimamizi endelevu wa mchanga. Haya yaliidhinishwa na UNEA katika mwaka wa 2022 kupitia azimio jipya kwa kichwa cha Vipengele vya mazingira vya usimamizi wa madini na metali, lililoithishwa na nchi zote wanachama.    

Pakua ripoti hiyo na picha za kiwango cha juu ili kuandamana na visa vya habari hapa. 

MAKALA KWA WAHARIRI  

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa  

UNEP ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira duniani. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.    

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:  

 Alejandro Laguna, Afisa wa Mawaliano, UNEP Ofisi ya Ulaya, +41 766910848,
Pascal Peduzzi, Mkurugenzi,  GRID-Geneva, UNEP, +41 (0)22 917 82 37,