Duncan Moore, UNEP
30 Oct 2023 Toleo la habari Kushughulikia kemikali na uchafuzi

Tuzo la Umoja wa Mataifa la ngazi ya juu zaidi linawatuza wanatoa masuluhisho bunifu ya kukomesha uchafuzi wa plastiki

Nairobi, Octoba 30, 2023 – Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) leo lilitangaza Mabingwa wa Dunia wa mwaka wa 2023, kwa heshima ya meya wa jiji, shirika lisilo la biashara, Shirika la kijamii, mradi wa serikali na baraza la utafiti kwa masuluhisho yao bunifu na hatua zao za mabadiliko chanya ya kukabiliana na uchafuzi wa plastiki.

Tangu kuzinduliwa kwake katika mwaka wa 2005,  tuzo la Mabingwa wa Dunia linalotolewa kila mwaka, limetolewa kwa watu walio msitari mbele kuanzisha juhudi za kulinda watu na sayari. Ni tuzo la Umoja wa Mataifa la ngazi ya juu zaidi linalotolewa kwa heshima ya mazingira. Ikijunuisha Mabingwa tano wa mwaka huu, tuzo hili limetolewa kwa washindi 116: viongozi wa dunia 27, watu binafsi 70 na mashirika 19. UNEP ilipokea mapendekezo 2,500 katika awamu hii, na kuwa mwaka wa tatu mfululizo wa kupokea mapendekezo mengi zaidi.

"Uchafuzi wa plastiki ni jambo linalohusiana sana na changamoto za aina tatu duniani. "Ili kuwa na afya njema na sayari thabiti, ni sharti tukomeshe uchafuzi wa plastiki. Hii inahitaji mabadiliko kamili, ili kupunguza kiasi cha plastiki zinazozalishwa na kuondoa plastiki inayotumika mara moja; na kuanza kutumia mifumo ya kutumia bidhaa tena na tena na njia mbadala zinazoepuka athari mbaya kwa mazingira na kwa jamii tunazoshuhudia kutokana na uchafuzi wa plastiki,” alisema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP. “Mazungumzo ya kuunda chombo cha kisheria cha kimataifa kuhusu uchafuzi wa plastiki yanapoendelea, Mabingwa wa Dunia mwaka huu wanaonyesha kuwa kuna masuluhisho bunifu yanayoweza kututia moyo kutafakari kuhusu uhusiano wetu na plastiki.

Washindi wa UNEP wa mwaka wa 2023 wa tuzo la Mabingwa wa Dunia ni:

  • Meya Josefina Belmonte wa Jiji la Quezon, Ufilipino, aliyetuzwa katika kitengo cha Uongozi Unaozingatia Sera, anaendesha za kujali mazingira na jamii kupitia msururu wa sera za kukabiliana na janga la mabadiliko ya tabianchi, kukomesha uchafuzi wa plastiki na kutochafua maeneo la miji. Juhudi zake ni pamoja na kupiga marufuku plastiki inayotumika mara moja, mpango wa biashara unaoshughulikia uchafuzi wa plastiki, vituo vya kujaza vitu muhimu vya kila siku na upiganiaji wa uundaji wa sera dhabiti za kimataifa kuhusu plastiki.
  • Wakfu wa Ellen MacArthur (Uingereza), unaotuzwa katika kitengo cha Motisha na Kuchukua Hatua, umetekeleza wajibu katika kujingatia mzunguko mjima, ikijumuisha wa plastiki.Wakfu huo umechapisha ripoti na kuanzisha mitandao ya wafanya maamuzi katika sekta ya kibinafsi na ya umma, pamoja na wasomi, ili kukuza mipango ya masuluhisho yanayozingatia mzunguko mzima kwa janga la mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa bayoanuai, uchafuzi wa plastiki na kadhalika. Unaongoza Ahadi Ulimwenguni pamoja na UNEP.
  • Blue Circle (China), inatuzwa katika kitengo cha Maono ya Ujasiriamali, hutumia teknolojia ya blockchain na mtandao wa mambo kufuata na kufuatilia mzunguko mzima wa uchafuzi wa plastiki - kuanzia kwa ukusanyaji hadi kuunda vitu vipya, kuitengeneza upya na kuiuza tena. Imekusanya zaidi ya tani 10,700 za uchafu kutoka baharini, na kuifanya kuwa programu kubwa zaidi ya Uchina ya taka za plastiki baharini. 
  • José Manuel Moller (Chile), anayetuzwa pia katika kitengo cha Maono ya Ujasiriamali, ni mwanzilishi wa Algramo, shirika la jamii linalojitolea kutoa huduma za kujaza tena vitu vilivyotumika hali inayopunguza uchafuzi wa plastiki na kupunguza gharama za vitu vinavyotumika kila siku. Moller pia anafanya kazi ya kuzuia, kupunguza na kushughulikia taka kwa njia endelevu kupitia nafasi yake kama Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Umoja wa Mataifa ya Watu Mashuhuri ya kutozalisha taka kabisa, mpango ulioanzishwa Machi mwaka wa 2023.
  • Baraza la Utafiti wa Kisayansi na Viwanda (Afrika Kusini), linatuzwa katika kitengo cha Sayansi na Ubunifu, hutumia teknolojia ya kisasa na utafiti wa fani mbalimbali kuendeleza uvumbuzi wa kukabiliana na uchafuzi wa plastiki na masuala mengine. Ni mwanzilishi katika kutambua njia mbadala endelevu za kushughulikia plastiki ya kawaida, na kutoa fursa kwa viwanda vya eneo vya kutengeneza bidhaa na kukuza uchumi na kutathini uwezekano wa plastiki kuoza.

https://youtu.be/Q1B4HBASlsw

Plastiki imebadilisha maisha ya kila siku na kutoa manufaa mengi kwa jamii. Hata hivyo, binadamu hutengeneza takribani tani milioni 430 za plastiki kila mwaka, thuluthi mbili ni vitu ambavyo hufanywa taka baada ya muda mchache. Mazoea yetu ya kutumia plastiki inayotumika kwa muda mfupi yamepelekea kile kinatajwa na wataalamu kuwa janga kwa mazingira.

Kila mwaka, hadi tani milioni 23 za taka ya plastiki hujikuta kwenye mifumo ya ekolojia ya majini na kuchafua maziwa, mito na bahari. Kufikia mwaka wa 2040, uzalishaji wa hewa ya ukaa unaohusishwa na uzalishaji, matumizi na utupaji wa plastiki za kawaida kutokana na fueli ya visukuku unaweza kuchangia moja kwa tano ya uzalishaji wa gesi ya ukaa chini cha malengo kabambe ya Mkataba wa Paris wa Mabadiliko ya tabianchi. Kemikali ndani ya plastiki zinaweza kusababisha matatizo ya kiafya kwa binadamu.

Wataalamu wa #KomeshaUchafuziWaPlastiki, wanasema binadamu lazima wapunguze na kukomesha plastiki isiyohitajika na inayosababisha matatizo, watafute njia mbadala zinazojali mazingira kwa bidhaa hii, wabuni mifumo bunifu ya kutumia tena plastiki na kutumia kile kinachojulikana kama mbinu ya kukabiliana na mzunguko mzima wa uchafuzi wa plastiki.

 

MAKALA KWA WAHARIRI

Kuhusu Tuzo la UNEP la Mabingwa wa Dunia
Tuzo la UNEP la  Mabingwa wa Dunia hutuza watu binafsi, makundi na mashirika ambayo huchukua hatua za kusababisha mabadiliko chanya kwa mazingira. Tuzo linalotolewa kila mwaka la Mabingwa wa Dunia ni tuzo la Umoja wa Mataifa la ngazi ya juu zaidi linalotolewa kwa heshima ya mazingira. #MabingwaWaDunia

Kuhusu kampeni ya #KomeshaUchafuzi
Ili kupambana na athari mbaya za uchafuzi kwa jamii, UNEP ilizindua #KomeshaUchafuzi, mkakati utakaopelekea hatua za dharura, za kiwango kikubwa na zilizoratibiwa dhidi ya uchafuzi wa hewa, ardhi na maji. Mkakati huu unaangazia athari za uchafuzi kwa mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa bayoanuai, na afya ya binadamu. Kupitia ujumbe unaotegemea sayansi, kampeni hii inaonyesha jinsi kuhamia sayari isiyo na uchafuzi ni muhimu kwa vizazi vijavyo.

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:
Kitengo cha Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa