Abdullah Ibrahim Alissa amesimama kwenye eneo lililo na mawe katika Mbuga ya Taifa ya Thadiq, eneo kubwa la ardhi kame kaskazini mwa Riyadh, mji mkuu wa Ufalme wa Saudi Arabia.
Chini ya Alissa, msimamizi wa mbuga hiyo, kuna mitaro mikubwa iliyo na vichaka na miti midogo iliyopandwa kwa uangalifu, iliyostawi ya kijani kibichi ambayo imegeuza mahali hapa kutoka kwa jangwa hadi mahali pa mazingira yanayopendeza.
"Nilikulia katika eneo hili, na tangu utotoni nililiona likiharibika na kuwa jangwa," Alissa anasema. "[Lakini] kupitia miradi ya upandaji miti, ulinzi na utunzaji wake, eneo hili limebadilika kabisa."
Kuhuisha mbuga hii ya kilomita za mraba 600, maarufu kwa mabonde yake makubwa, ilihusisha kupanda miti 250,000 na vichaka milioni 1. Wafanyakazi pia walijenga mabwawa yenye mitaro ili kupata maji machache ya mvua ambayo hujiri kwa nadra eneo hilo.
Kuboresha Mbuga ya Kitaifa ya Thadiq ni sehemu ya mpango mpana wa Saudi Arabia wa kurejesha miti katika maeneo makubwa ya jangwa ndani na nje ya nchi. Kichocheo chake ni kukabiliana na ukame, kuenea kwa majangwa, na uharibifu wa ardhi, ambavyo vinatishia nchi Asia Magharibi na Afrika Kaskazini kote.
Robo tatu ya ardhi inayofaa kutumika kwa kilimo katika eneo hili tayari imeharibiwa, na asilimia 60 ya watu tayari wanakabiliwa na uhaba wa maji, idadi inayotarajiwa kuongezeka kufikia mwaka wa 2050.
"Ardhi ni nguzo muhimu ya maisha, na pamoja na bahari na mazingira, ni muhimu kuendeleza maisha katika Dunia hii," anasema Osama Ibrahim Faqeeha, Naibu Waziri wa Mazingira wa Saudi Arabia.
Tarehe 5 Juni, Saudi Arabia itakuwa mwenyeji wa Siku ya Mazingira Duniani Mwaka wa 2024, maadhimisho ya kila mwaka ya sayari ambayo mwaka huu yanaangazia kuenea kwa majangwa, uharibifu wa ardhi na kustahimili ukame.
Zaidi ya hekta bilioni 2 za ardhi duniani zimeharibiwa, na kuathiri nusu ya idadi ya watu wote duniani, na kutishia viumbe wengi.
Kwa kukabiliwa na ukame mkali zaidi na wa kipindi kirefu, dhoruba za mchanga na na joto kuongezeka, kutafuta njia za kuzuia ardhi iliokauka kuwa jangwa, vyanzo vya maji safi kutoyeyuka, na udongo wenye rutuba kugeuka na kuwa vumbi, ni muhimu sasa, wanasema wataalam.
Saudi Arabia, ambapo maendeleo ya haraka na ongezeko la ulishaji wa mifugo vimesababisha uharibifu wa ardhi, imetoa kipaumbele kwa kukabiliana na majangwa.
Mpango uliozinduliwa Machi mwaka wa 2021, Mpango wa Kijani wa Saudia unalenga kugeuza asilimia 30 ya ardhi ya Saudi Arabia kuwa hifadhi za kiasili, kupanda miti bilioni 10 na kuboresha hekta milioni 40 za ardhi iliyoharibiwa.
"Lengo la nchi ni kupanda miti milioni 400 kufikia mwaka wa 2030," anasema Khaled Alabdulkader, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kitaifa cha Maendeleo ya Kukuza Mimea na Kupambana na Kuenea kwa MaJangwa cha Saudi Arabia.
"Mpango wa Saudi Green unaonyesha uwezo mkubwa wa mtaji wa kitamaduni na hekima ya kiasili ya kusimamia mazingira asilia," anasema Susan Gardner, Mkurugenzi wa Kitengo cha Mifumo ya Ekolojia katika Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP). "Mbinu kama hizo, zilizo na msingi wa kiasili na zilizoundwa kutegemea eneo, ni muhimu sana katika eneo ambalo linakabiliwa na changamoto nyingi zinazopelekea uharibifu wa ardhi na kuenea kwa majangwa."
Kupitia kwa Mpango wa Kijani wa Mashariki ya Kati, Saudi Arabia inaongoza juhudi za kupanda miti zaidi ya bilioni 40 katika eneo lote na lengo la kupunguza mmomonyoko wa udongo, kulinda ubayoanuai, na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi. Lengo la kupanda miti bilioni 50 kwa pamoja linawakilisha asilimia tano ya lengo la kimataifa la upandaji miti, na ni sawa na kuboresha hekta milioni 200 za ardhi iliyoharibiwa.
Saudi Arabia pia imeshirikiana na Kundi la mataifa 20 na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kukabiliana na Kuenea kwa majangwa (UNCCD) kuzindua Mpango wa Ardhi wa G20, unaolenga kupunguza uharibifu wa ardhi kwa asilimia 50 kufikia mwaka wa 2040. Vilevile, Saudi Arabia itakuwa mwenyeji wa Kongamano la 16 la Nchi Wanachama wa UNCCD, linaloonekana sana kama wakati muhimu katika juhudi za kimataifa za kukomesha uharibifu wa ardhi.
Kote duniani, nchi zimeahidi kuboresha hekta bilioni 1 za ardhi – eneo kubwa kuliko Uchina, chini ya Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia. Lakini ikiwa mwelekeo wa sasa utaendelea, hekta bilioni 1.5 zitahitaji kuboreshwa ili kufikia malengo ya mwaka wa 2030 ya kutokuwa na ubaguzi wowote kuhusiana na uharibifu wa ardhi.
"Shughuli za utunzaji na uboreshaji wa ardhi hupelekea matokeo chanya kwa bayoanuai pamoja na manufaa mengi kwa watu, ikiwa ni pamoja na maji na utoshelezaji wa chakula, afya ya umma na ustawi, kushughulikia na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi," anasema Gardner anayefanya kazi na UNEP.
Tukirudi katika Hifadhi ya Kitaifa ya Thadiq, Alissa na wahifadhi wengine wa mazingira wamefurahishwa na kurudi kwa ndege kwenye eneo hilo, eneo ambalo lilikuwa limeshuhudia kuhama kwa wanyama huku jangwa likizidi kuenea.
Takriban mitaro 100 ya maji inayoenea kama ngazi hadi chini ya mabonde, huteka maji ya mvua ili kuendelea kukuza vichaka na miche katika majira ya joto kali. Pia huzuia mvua nyingi za msimu wa baridi kusomba udongo mzuri.
"Tulirithi mitaro ya maji kutoka kwa babu zetu karibu miaka 400 iliyopita," anasema Alissa. "Tulitumia mbinu hii mbugani, na inafanya kazi nzuri katika kuongeza maji ya juu ya ardhi."
Kwa kuzingatia masuluhisho ya kiasili kuboresha ardhi iliyoharibika, mbuga hiyo imeendelea kukuza miti katika vitalu, na kupanda aina nyingi za kiasili.
"Natumai tunaweza imarisha kazi yetu na matokeo yetu maradufu, kuongeza upandaji miti na maeneo mengine kutuiga," Alissa anasema.
Siku ya Mazingira Duniani tarehe 5 Juni ni hafla kubwa zaidi ya kimataifa ya mazingira. Hafla inayoongozwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na kufanyika kila mwaka tangu mwaka wa 1973, hafla hii imekua hadi kuwa jukwaa kubwa zaidi duniani la kuhamasisha kuhusu mazingira, huku mamilioni ya watu kutoka pembe zote za dunia wakishiriki ili kutunza sayari. Siku ya Mazingira Duniani mwaka wa 2024 itaangazia uboreshaji wa ardhi, kuenea kwa majangwa na kustahimili ukame.